Alhamisi. 21 Novemba. 2024
feature-top
Changamoto ya wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum: Utaifa, Ubaguzi na Chuki dhidi ya wageni

Misimamo mikali ya kisiasa inayofumbatwa katika utaifa usiokuwa na mvuto wala mashiko kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; ubaguzi na chuki dhidi ya wageni ni kati ya changamoto zinazoendelea kutishia mpango mkakati wa Kanisa katika huduma kwa wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum. Kuna baadhi ya viongozi wanatafuta umaarufu kwa ubabe!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani pamoja na kuibuka kwa misimamo mikali ya kisiasa inayofumbatwa katika utaifa usiokuwa na mvuto wala mashiko kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; ubaguzi na chuki dhidi ya wageni ni kati ya changamoto zinazoendelea kutishia mpango mkakati wa Kanisa katika huduma kwa wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum. Kuna baadhi ya viongozi wa kisiasa wanaotaka umaarufu wa kisiasa kwa kuonesha ubabe dhidi ya wakimbizi na wahamiaji.

Hii ni sehemu ya hotuba elekezi iliyotolewa hivi karibuni na Monsinyo Bruno Marie Duffè Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu na fungamani ya binadamu kwenye Chuo Kikuu cha “Santa Caterina wa Siena” huko Pavia, nchini Italia. Anasema, watu wakiangalia kwa undani kabisa watagundua kwamba, kila binadamu ni mkimbizi au mhamiaji, anayecharika usiku na mchana ili kutafuta chemchemi ya maisha bora zaidi, changamoto na mwaliko wa kuondokana na mawazo mgando yanayojikita katika sera za kibaguzi na chuki dhidi ya wageni, hasa wakimbizi na wahamiaji.

Monsinyo Bruno Marie Duffè anasema, kuna haja ya kuwa na mwelekeo na mwono mpya mintarafu changamoto mamboleo, kwa kuandika upya historia ya mwanadamu inayofumbatwa katika: haki msingi za binadamu, utu, heshima, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Wakimbizi na wahamiaji ni watu wanaotafuta: hifadhi, usalama na maisha bora zaidi. Ni watu wanaotaka kuboresha maisha yao kwa kuondokana na umaskini wa hali na kipato na matokeo yake kama ilivyokuwa katika historia, nao wanaunda familia mpya ya binadamu. Hawa ni watu wenye utajiri wa maisha ya kiroho na kiutu, wanapopewa nafasi wanachangia pia ustawi na maendeleo ya wenyeji wao.

Ikumbukwe kwamba, kuna nchi ambazo ustawi na maendeleo yake yametokana na jasho la wakimbizi na wahamiaji, lakini leo hii, zimekuwa ni nchi za kwanza zinazoweka vikwazo dhidi ya wahamiaji na wakimbizi na kusahau kwamba, historia ni mwalimu wa maisha “historia magistra vitae”! Mshikamano wa umoja, udugu na upendo, unaweza kugeuza wasi wasi na hofu dhidi ya wageni na kuwa ni mwanzo wa cheche za furaha ya Injili na matumaini kwa watu wote! Wakimbizi na wahamiaji wanaobisha hodi katika malango ya nchi tajiri ni sura na mfano wa Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu.

Hofu ya kumezwa na wageni na hali ya kukosa utambulisho wa kitaifa ni hoja zisizo na mashiko hata kidogo. Katika ulimwengu wa utandawazi, Baba Mtakatifu Francisko anasema, watu wanapaswa kuthubutu kujenga madaraja yanayowakutanisha watu: kitamaduni, kidini na kiutu, kwa kutambua kwamba, wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na wala tofauti zao msingi zisiwe ni kisingizio cha vita, kinzani na mipasuko ya kijamii na kifamilia! Hakuna kitu kinachoweza kupotea kwa njia ya ukarimu hasa katika ulimwengu wa utandawazi ambao umegeuka kuwa kama kijiji.

Utandawazi unapaswa kujikita katika huruma ili kukuza na kudumisha mshikamano wa upendo na ukarimu, tayari kupyaisha mitazamo na malengo ya maisha. Vinginevyo, ulimwengu utaendelea kutawaliwa na sera za kibaguzi na chuki dhidi ya wageni kama vile wakimbizi na wahamiaji na hivyo kuwafungia malango ya matumaini ya maisha mapya, matokeo yake ni kuwaacha watu hawa watumbukie katika ombwe la kifo, biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo. Historia ya binadamu inafumbatwa katika hija ya kukutana na wengine, kugundua maeneo mapya na hatimaye kuwa na mang’amuzi pamoja na matumaini mapya yanayojielekeza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, uchungu na fadhaa ya wanadamu wa nyakati zetu, hasa ya maskini na ya wale wote wanaoteswa, yote ni furaha na matumaini, uchungu na fadhaa ya wafuasi wa Kristo pia.

Hii ni changamoto ya kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa kidugu, kwa kusikiliza na hatimaye, kujibu kilio cha watu wanaoteseka katika ulimwengu mamboleo. Mafundisho Jamii ya Kanisa ni dira na mwongozo wa kukuza na kudumisha utu na heshima ya binadamu; bila kusahau haki zake msingi. Maskini daima ni amana na utajiri wa Kanisa kama wanavyokaza kusema, Mababa wa Kanisa. Hizi ni kanuni msingi zinazofumbatwa katika maadili, utu wema na upendo kwa Mungu na jirani.

Waamini wajenge umoja na mshikamano na watu wote bila ubaguzi. Ikumbukwe kwamba, siasa safi ni chombo cha huduma ya haki, amani, ustawi na maendeleo fungamani ya binadamu! Waamini wanahamasishwa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani, unaokita mizizi yake katika: haki, amani na upendo; mambo yanayodai wongofu wa ndani unaotambua sura na mfano wa Mungu katika kila mwanadamu!

Maoni


Ingia utoe maoni