Jumatano. 04 Desemba. 2024
feature-top
UNO: Athari za mabadiliko ya tabianchi ni changamoto kubwa Barani Afrika!

Kama Bara la Afrika halitajizatiti kikamilifu kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote, athari zake ni kubwa sana! Hadi sasa joto limepanda kiasi cha kutishia maisha, kuna ukame wa kukithiri na kwamba, katika kipindi cha miaka 30 ijayo, watu zaidi ya milioni 86 wataathirika kutokana na kupanda kwa kiwango cha joto duniani. Hali hii, itahatarisha uchumi, usawa na mafungamano ya kijamii.

Athari za mabadiliko ya tabianchi ni changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inasikiliza na kujibu kilio cha maskini kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wanaoendelea kuteseka kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi, changamoto changamani, inayopaswa kuvaliwa njuga na wadau wote! Uchafuzi wa mazingira unafifisha uzalishaji wa bidhaa na utoaji wa huduma kwa jamii; unahatarisha misingi ya haki, amani na maridhiano na kwamba, rasilimali za nchi zinakwapuliwa bila utaratibu na matokeo yake ni madhara makubwa kwa siku za usoni. Haki jamii ni muhimu sana katika kujenga na kudumisha mafungamano ya kijamii katika medani mbali mbali za maisha.

Bwana Antonio Guterres, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anasema, athari za mabadiliko ya tabianchi Barani Afrika ni kubwa, kiasi cha kutishia: usalama, amani, maisha na mustakabali wa Bara la Afrika kwa siku za usoni. Kama Bara la Afrika halitajizatiti kikamilifu kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote, athari zake ni kubwa sana! Hadi sasa joto limepanda kiasi cha kutishia maisha, kuna ukame wa kukithiri na kwamba, katika kipindi cha miaka 30 ijayo, watu zaidi ya milioni 86 wataathirika sana kutokana na kupanda kwa kiwango cha joto duniani. Hali hii, itahatarisha uchumi, usawa na mafungamano ya kijamii Barani Afrika.

Maeneo yatakayoathirika zaidi kadiri ya takwimu za Umoja wa Mataifa ni: Eneo lote Kusini mwa Jangwa la Sahara, Bahari ya Shamu, Ukanda wa Saheli pamoja na nchi ambazo ziko Pwani ya Pembe ya Afrika. Kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi kutokana na ongezeko la joto Barani Afrika, watu milioni 30-60 watalazimika kuzikimbia nchi zao ili kutafuta usalama, hifadhi na maisha bora zaidi. Kutokana na changamoto zote hizi, Bwana Antonio Guterres, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anasema kuna haja kwa Bara la Afrika kuhakikisha kwamba, linajizatiti katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Katika muktadha huo huo wa majanga yatokanayo na mabadiliko ya tabia nchi, imeelezwa kuwa licha ya bara la Afrika kukabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa rasilimali fedha na teknolojia  katika kupambana na madhara ya mabadiliko ya tabia nchi bara hilo lazima lijitutumue ili kupunguza madhara hayo. Wachunguzi wa mambo wanasema, rasilimali na utajiri wa nchi vinapaswa kutumiwa vyema kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, kuliko mtindo wa sasa ambao sehemu kubwa ya utajiri na rasilimali za dunia zinamilikiwa na watu wachache ndani ya jamii kwa ajili ya mafao yao binafsi!

Uchafuzi wa mazingira ni suala la kimaadili linalopaswa kuvaliwa njuga na waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema. Haya ni mapambano endelevu kama ilivyo kwa janga la Ukimwi na balaa la njaa duniani. Hapa kunahitajika wongofu wa kiekolojia, uthabiti wa kanuni maadili na utu wema na ujasiri unaomwilishwa katika uongozi bora unaozingatia sheria, kanuni na taratibu. Lengo ni kudumisha misingi ya haki, amani na mchakato wa maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu.


Maoni


Ingia utoe maoni