Jumamosi. 23 Novemba. 2024
feature-top
Mtakatifu Padre Pio wa Pietrelcina ni mfano bora wa kuigwa kwa kulipenda na kuliheshimu Kanisa licha ya udhaifu wa watoto wake!

Kanisa ni takatifu kwa sababu muasisi wake ni Kristo Yesu, Nafsi ya Pili katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Lakini, Mama Kanisa anao watoto wake ambao wanaogelea katika lindi la dhambi! Mtakatifu Padre Pio alilipenda Kanisa, kiasi hata akapewa neema ya kusamehe na kusahau! Haiwezekani kuendelea kuishi ndani ya Kanisa kwa kulishutumu kila kukicha kama anavyofanya Shetani, Ibilisi!

Familia ya Mungu kutoka Jimbo Katoliki la Benevento, Italia, ikiwa imeungana na viongozi wa Kanisa na Serikali, Jumatano, tarehe 20 Februari 2019, imekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, kama alama ya shukrani kwa hija ya kitume, ambayo Baba Mtakatifu aliifanya Jimboni mwao kunako tarehe 17 Machi 2018, kama sehemu ya maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka 50 tangu Padre Pio alipopata Madonda Matakatifu mwilini mwake na miaka 100 tangu alipofariki dunia.

Baba Mtakatifu Francisko ametumia fursa hii kuwashukuru wote kwa moyo wao wa ukarimu waliomwonjesha siku ile, akapata bahati ya kukutana na kuzungumza na wagonjwa mbali mbali na kwamba, ni tukio ambalo limeacha chapa ya kudumu katika moyo wake. Hili ni tukio ambalo lilikuwa na umuhimu wa pekee katika maisha na utume wa Kanisa; ikawa ni nafasi ya kuweza kufafanua na kuzama zaidi katika maisha ya kiimani mintarafu Mafundisho ya Mtakatifu Padre Pio wa Pietrelcina: maisha ya sala, unyenyekevu na hekima! Huyu ni Mtakatifu aliyekuwa na imani na matumaini thabiti kwa Mwenyezi Mungu; akajitoa na kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya watu wake; akalipenda na kuliheshimu Kanisa licha ya matatizo na changamoto zake!

Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, Kanisa ni takatifu kwa sababu muasisi wake ni Kristo Yesu, Nafsi ya Pili katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Lakini, Mama Kanisa anao watoto wake ambao wanaogelea katika lindi la dhambi! Mtakatifu Padre Pio alilipenda Kanisa, kiasi hata akapewa neema ya kusamehe na kusahau! Haiwezekani kuendelea kuishi ndani ya Kanisa kwa kulishutumu kila kukicha kama anavyofanya Shetani, Ibilisi! Waamini wawe na ujasiri wa kuonesha udhaifu na mapungufu ya Kanisa, lakini pia walipende na kuliheshimu Kanisa. Makosa yarekebishwe kwa toba na wongofu wa ndani ili Kanisa lisonge mbele!

Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumpenda na kumkaribisha Mwenyezi Mungu katika maisha yao, ili kwa njia ya upendo huo, aweze kuwaletea maisha mapya, kwa kujisadaka zaidi kwa ajili ya maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii! Upendo wa Kimungu unasaidia mchakato wa ujenzi wa dunia inayosimikwa katika haki na mshikamano. Kwa mfano na maombezi ya Mtakatifu Padre Pio, waamini wasichoke kujiaminisha kwa Kristo Yesu ili kutangaza na kushuhudia upendo, wema na huruma yake isiyokuwa na kifani!

Baba Mtakatifu anawatuma waamini kumshuhudia Kristo kama alivyofanya Mtakatifu Francisko wa Assisi, kwa kuishi na kutenda kama Wakristo; kwa kujenga na kudumisha urafiki na upendo kati ya watu, ili kufyekelea mbali “ndago za uadui na roho mbaya” ili hatimaye, kukuza na kudumisha udugu badala ya vita na mipasuko ya kijamii!


Maoni


Ingia utoe maoni