Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili, tarehe 17 Februari 2019 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, amewaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, ili kusali kwa ajili ya kuombea Mkutano wa Kanisa kuhusu Ulinzi kwa Watoto Wadogo utakaofanyika mjini Vatican kuanzia Alhamisi tarehe 21 hadi Jumapili tarehe 24 Februari 2019. Huu ni mkutano unaowajumuisha Marais wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki kutoka sehemu mbali mbali za dunia, pamoja na viongozi waandamizi wa Kanisa Katoliki, ili kwa pamoja kuweza kupembua kwa kina na mapana kuhusu ulinzi wa watoto ndani ya Kanisa.
Baba Mtakifu anakaza kusema, ameitisha mkutano huu kama kielelezo makini cha wajibu wa kichungaji ili kuweza kukabiliana na changamoto hii nyeti katika ulimwengu mamboleo. Lengo ni kutoa katekesi kwa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali za dunia, ili Maaskofu waweze kutambua madhara ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo. Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, watu walionyanyaswa kijinsia wanakabiliana na hali ngumu sana katika maisha yao: kiroho na kiutu. Maaskofu wataweza kusikiliza shuhuda za waathirika wa nyanyaso za kijinsia.
Padre Hans Zollner, mjumbe wa Kamati kuu ya Maandalizi ya Mkutano huu anasema, Kanisa linataka kujenga imani na matumaini; kwa kuamsha dhamiri za watu kuhusu umuhimu wa kuwalinda watoto wadogo, dhamana na wajibu kwa watu wote. Hii ni sehemu ya utekelezaji wa mbinu mkakati wa “Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa”. Ikumbukwe kwamba, nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo ni uhalifu wa hali ya juu kabisa unaoharibu maisha, utu na heshima ya watoto wadogo, kiasi cha kusababisha athari kubwa sana kwa watu!
Kwa upande wake, Kardinali Seàn O’Malley, Mwenyekiti wa Tume ya Kipapa ya Kulinda Watoto Wadogo, PCPM, anasisitiza kwamba, mkutano huu utaongozwa na mambo makuu matatu: uwajibikaji, dhamana ya uwajibikaji; ukweli na uwazi. Kamati kuu imetuma barua kwa washiriki wa mkutano huu pamoja na maswali dodoso yatakayowawezesha kushiriki kikamilifu! Tume ya Kipapa ya Kulinda Watoto Wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia iliundwa kunako mwaka 2014 inaendelea kujikita katika kuwasililiza waathirika wa nyanyaso za kijinsia; kutoa elimu na majiundo makini; kukazia sheria kanuni na taratibu zinazopaswa kufuatwa, ili kujenga mazingira salama kwa watoto.
Pamoja na mambo mengine, Tume hii inatoa mwongozo wa kuwalinda watoto wadogo; mchakato wa uponyaji kwa watu walioathirika na nyanyaso za kijinsia; malezi na majiundo makini kwa Majandokasisi wanaojiandaa kwa ajili ya kupokea Daraja Takatifu, Watawa pamoja na viongozi wa Kanisa katika masuala ya elimu. Tume hii ina dhamana ya kutoa elimu kwa familia na jumuiya za kikristo, kwa kujikita katika taalimungu na tasaufi; sheria, kanuni na taratibu za Kanisa pamoja na sheria za kiraia.
Maoni
Ingia utoe maoni