Heri za Mlimani kama zilivyoandikwa na Mwinjili Luka zimegawanyika katika sehemu kuu nne zinazofumbatwa katika “Heri na Ole”, mwaliko na changamoto kwa waamini kuyaangalia matukio ya ulimwengu huu kwa jicho la imani pamoja na kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu. Huu ni mwaliko wa kupambana na malimwengu, ili kuweza kupata furaha ya kweli inayomwezesha mwamini kuwa karibu zaidi na Mwenyezi Mungu kwa kuonesha upendo kwa Mungu na jirani! Yesu anasema heri maskini, wenye njaa, wenye kulia na kudhulumiwa. Kwa upande mwingine anasema, Ole wenu: matajiri, watu walioshiba, wale wanaocheka na kusifiwa na watu.
Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili, tarehe 17 Februari 2019, wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, Mwenyezi Mungu yuko karibu na wale wote wanaoteseka na kusumbuka na kwamba, iko siku atawakomboa kutoka katika utumwa wa maisha yao. Yesu anawaonya, wale wote waliobahatika kuwa na maisha mazuri hapa duniani, kuwa macho, ili kamwe wasielemewe na uchoyo na ubinafsi, bali wawe tayari kushirikishana na wengine utajiri waliokirimiwa na Mwenyezi Mungu kama kielelezo cha Injili ya upendo na mshikamano na kwamba, huu ndio muda wa kumwilisha upendo huu kati ya watu!
Mwinjili Luka anawaalika waamini kuzama zaidi katika imani, kwa kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu, ili kuvunjilia mbali vishawishi na tamaa za ulimwengu, tayari kumfungulia Mungu wa kweli na aliye hai, malango ya maisha! Leo hii kuna mambo yanayoonekana kuwa ni chemchemi ya furaha na mafanikio katika kipindi kifupi tu cha maisha; mambo yanayoweza kuwapatia watu mali na utajiri; hata miujiza ya kuponya na kuganga yale yasiyowezekana! Hapa kuna hatari kubwa kwa waamini kuteleza na kutumbukia katika dhambi ya kuabudu miungu dunia na kumwacha Mungu wa kweli. Dhana hii inaweza kuonekana kana kwamba, imepitwa na wakati, lakini anasema Baba Mtakatifu Francisko hii ni changamoto ya nyakati zote, hata katika ulimwengu mamboleo!
Ni katika muktadha huu, Kristo Yesu anatumia “Heri” na “Ole” ili kuwapatia nafasi wafuasi wake, ili waweze kuangalia ukweli kwa macho makavu! Watu wote wanaitwa kuwa na furaha, ikiwa kama watakuwa upande wa Mungu, kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wake, ili hatimaye, kuweza kupata furaha na maisha ya uzima wa milele. Watu watakuwa na furaha ya kweli, ikiwa kama watajisikia kuwa ni wahitaji mbele ya Mwenyezi Mungu; ikiwa kama watakuwa karibu na tayari kuwasaidia maskini, wanaoteseka na wale wanaokufa kwa baa la njaa na utapiamlo duniani. Baba Mtakatifu anawakumbusha waamini kwamba, mbele ya Mwenyezi Mungu, hata wao ni maskini, wanaoteseka na kufa kwa njaa na kiu.
Furaha ya kweli inapatikana pale ambapo waamini wanapotumia vyema mali na utajiri wa duniani hii kwa kushirikishana na jirani zao, changamoto na mwaliko kwa kila mwamini kuchunguza dhamiri yake kuhusu ukweli huu. Heri za Mlimani ni ujumbe makini unaowataka waamini kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu kwa kupambana fika na wale watu wanaouza “ndoto za mchana” kiasi cha kushindwa kuwakirimia matumaini. Kristo Yesu, anawakirimia waja wake, uwezo wa kuona ukweli wa mambo, kwa kuwaganga na kuwaponya ufinyu wa mawazo yanayoweza kuwatumbukiza na hatimaye, kumezwa na malimwengu.
Neno la Mungu linawahimiza waamini kutafuta kile kilicho kweli, chema na kizuri katika maisha, ili kuwatajirisha, kwa kuzima kiu na njaa ya maisha na hatimaye, kuwapatia utu na furaha ya kweli, yaani mambo msingi yanayomwezesha mwamini kupata utimilifu wa maisha. Mwishoni, Baba Mtakatifu anamwomba Bikira Maria, ili aweze kuwasaidia waamini kusikiliza kwa makini Injili ya Kristo, huku wakiwa na akili na nyoyo wazi, ili waweze kuzaa matunda yanayokusudiwa, kwa kuwa ni mashuhuda wa furaha ya kweli, ambayo kamwe haiwezi kumdanga mtu!
Maoni
Ingia utoe maoni