Jumanne. 03 Desemba. 2024
feature-top

Lengo la Mkutano wa Kanisa kuhusu Ulinzi kwa Watoto Wadogo kuanzia tarehe 21-24 Februari 2019 ni kutoa katekesi kwa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali za dunia, ili Maaskofu waweze kutambua madhara ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo. Watu walionyanyaswa kijinsia wanakabiliana na hali ngumu sana katika maisha yao: kiroho na kiutu.

Mkutano wa Viongozi wa Kanisa utakaofanyika mwezi Februari kuhusu dhamana ya kuwalinda watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia kwa kuwaundia mazingira bora zaidi ya malezi na makuzi yao, anasema Baba Mtakatifu Francisko ni changamoto iliyotolewa Baraza la Makardinali Washauri. Lengo ni kutoa katekesi kwa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali za dunia, ili Maaskofu waweze kutambua madhara ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo. Watu walionyanyaswa kijinsia wanakabiliana na hali ngumu sana katika maisha yao: kiroho na kiutu.

Jambo la pili, ni kuwasaidia Maaskofu kuchukua hatua makini mintarafu Sheria, Kanuni na Taratibu za Kanisa. Mkutano maalum wa viongozi wa Kanisa kwa ajili ya kuwalinda watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia utafanyika mjini Vatican kuanzia tarehe 21-24 Februari 2019. Kitakuwa ni kipindi cha sala, tafakari pamoja na kusikiliza ushuhuda, ili kutambua uzito wa kashfa hii katika maisha na utume wa Kanisa. Itakuwa ni nafasi ya kufanya toba, wongofu wa kichungaji na kuomba msamaha, tayari kuanza upya, ili kujikita katika mchakato wa utakatifu wa maisha.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, watu wasiwe na matarajio makubwa sana kwani kashfa kama hizi ni sehemu ya udhaifu wa binadamu unaoendelea kufanyika kwenye familia na jamii katika ujumla wake! Jambo la msingi kwa Mama Kanisa ni kuwa na protokali ya utekelezaji wa ulinzi kwa watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia! Mkutano huu utaongozwa na mambo makuu matatu: uwajibikaji, dhamana ya uwajibikaji; ukweli na uwazi. Kamati kuu imetuma barua kwa washiriki wa mkutano huu pamoja na maswali dodoso yatakayowawezesha kushiriki kikamilifu!

Padre  Hans Zollner, Rais wa Kituo cha Ulinzi kwa Watoto Wadogo, Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian ambaye pia ni mjumbe wa Kamati kuu inayoratibu mkutano maalum wa Kanisa kwa ajili ya kuwalinda watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia utakaofanyika mjini Vatican kuanzia tarehe 21-24 Februari 2019 anasema, kuna haja ya kufanya toba na wongofu wa ndani; pamoja na kubadili mwelekeo na mtazamo wa Kanisa kuhusu nyanyaso dhidi ya watoto wadogo sehemu mbali mbali za dunia.

Takwimu zinaonesha kwamba, kuna watoto zaidi ya milioni 80 wanaokumbana na nyanyaso za: kijinsia, kisaikolojia, kimwili, vita na vitendo vya kigaidi. Idadi kubwa ya watoto hawa ni changamoto kubwa inayopaswa kuamsha dhamiri nyofu, ili watu waweze kusimama kidete kuwalinda watoto wadogo. Jambo la msingi ni kufahamu uzito wa tatizo, ili kuweza kukabiliana kinagaubaga na kashfa hii ambayo imelichafua Kanisa katika maisha na utume wake. Hii ndiyo hatua ya kwanza ambayo Baba Mtakatifu anataka Kanisa kuitekeleza katika maisha na utume wake.

Kwa mara ya kwanza, viongozi wa Kanisa watapembua kwa kina na mapana mbinu mkakati wa kuwalinda watoto wadogo pamoja na kuanzisha miundo mbinu ya kimataifa itakayoshughulikia nyanyaso hizi. Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kushiriki kikamilifu katika mkutano huu. Kadiri ya ratiba elekezi, siku ya kwanza wajumbe watafanya tafakari ya kina kuhusu wajibu wa Askofu mahalia: kichungaji na kisheria. Siku ya Pili: Ni Askofu mahalia anawajibika kwa na nani: hapa ni mahali pa kuangalia mfumo mzima, taratibu na kanuni katika mchakato mzima wa utekelezaji wake. Hapa umuhimu wa dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa unapaswa kuzingatiwa.

Siku ya tatu, viongozi wa Kanisa watajikita katika dhana ya ukweli na uwazi ndani ya Kanisa, Serikali na kwa watu wa Mungu katika ujumla wao! Changamoto kubwa hapa ni mchakato wa Kanisa kujikita katika toba na wongofu wa ndani, tayari kubadili mwelekeo na mtazamo kuhusu kashfa ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo. Wajumbe watapata nafasi ya kusikiliza kwa makini shuhuda za baadhi ya waathirika wa wa nyanyaso za kijinsia! Hii ni kazi ambayo Maaskofu wametakiwa kuifanya katika Nchi zao, kabla ya kuanza kuja hapa mjini Vatican kushiriki katika mkutano huu. Maaskofu wanahamasishwa: kusikiliza kilio, kuangalia mateso na mahangaiko ya waathirika; ili hatimaye, waweze kuguswa na madonda makubwa wanayobeba mioyoni mwao.

Katika hali na mazingira kama haya, kamwe mtu hawezi kubaki bila kuguswa katika undani wa maisha na utume wake. Hii ni hatua ya kwanza katika mchakato mzima wa safari ambayo iko mbele ya maisha na utume wa Kanisa. Kuhusu kashfa ya nyanyaso za kijinsia, Kanisa linapaswa kusimama kidete kwa kuweka mbinu mkakati ili kuwaundia watoto mazingira safi ya malezi na makuzi yao.


Maoni


Ingia utoe maoni