Alhamisi. 21 Novemba. 2024
feature-top
Askofu Filbert Felician Mhasi, anawekwa wakfu na kusimikwa rasmi tarehe 17 Februari 2019 huko Jimboni Tunduru-Masasi.

Katika Ibada ya Masifu ya jioni, Askofu mteule, atakabidhiwa funguo za Kanisa kuu, ataonesha hati za uteuzi, atakula kiapo cha utii na uaminifu, ataungama kanuni ya imani. Katika Ibada ya Misa Takatifu ya kuwekwa wakfu, Askofu mteule, atapewa pete, alama ya uaminifu, dhamana ya kulilinda Kanisa Takatifu, bibi harusi wa Mwenyezi Mungu kwa imani nyoofu na maisha matakatifu.

Askofu Flavian Matindi Kassala, Makamu wa Rais Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania anawaalika waamini Jimbo Katoliki la Tunduru-Masasi kumpokea kwa ukarimu na upendo Askofu wao mpya Filbert Felician Mhasi, kama sehemu ya mapenzi na mpango wa Mungu, ili kweli Mwenyezi Mungu aabudiwe na mwanadamu apate wokovu sanjari na kuendeleza mchakato wa uinjilishaji mpya unaogusa mahitaji msingi ya watu wa Mungu, Kusini mwa Tanzania. Askofu Kassala anaongoza msafara wa Maaskofu kuelekea kwenye sherehe ya kumweka wakfu Askofu mteule Filbert Felician Mhasi, inayofanyika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Francisko Xsaveri, Jimbo Katoliki la Tunduru-Masasi, hapo tarehe 17 Februari 2019.

Tukio hili, linatanguliwa kwa Ibada ya Masifu ya Jioni, inayoadhimishwa, Jumamosi jioni tarehe 16 Februari 2019. Katika Ibada hii, Askofu mteule, atakabidhiwa funguo za Kanisa kuu, ataonesha hati za uteuzi kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko, atakula kiapo cha utii na uaminifu, ataungama kanuni ya imani. Katika Ibada ya Misa Takatifu ya kuwekwa wakfu, Askofu mteule, atapewa pete, alama ya uaminifu, dhamana ya kulilinda Kanisa Takatifu, bibi harusi wa Mwenyezi Mungu kwa imani nyoofu na maisha matakatifu. Atakabidhiwa Mitra, alama ya utakatifu unaong’aa na kama kielelezo cha mchungaji mkuu. Askofu pia atakabidhiwa Fimbo ya kichungaji, alama ya huduma ya kichungaji.

Itakumbukwa kwamba, Askofu Filbert Felician Mhasi alizaliwa tarehe 30 Novemba 1970, Biro Jimboni Mahenge. Alipata elimu yake ya sekondari katika Seminari ndogo ya Mtakatifu Francis, Kasita kati ya mwaka 1986-1992. Baadaye alikwenda katika Seminari kuu ya Mama wa Malaika, Kibosho Jimbo Katoliki la Moshi kwa ajili ya malezi na masomo ya Falsafa kati ya mwaka 1993-1995. Tangu Mwaka 1995-1998 alipata mafunzo ya Kitaalimungu katika Seminari kuu ya Mtakatifu Paulo Kipalapala Jimbo kuu la Tabora. Alipewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 3 Julai 2001 Jimboni Mahenge. Baada ya kupadrishwa, alipelekwa masomoni katika Chuo cha Kikatoliki Mwenge, Jimbo Katoliki la Moshi mwaka 2001-2003, ambako alitunukiwa shahada ya Elimu.

Kati ya mwaka 2003-2004 alikuwa Kaimu Gombera, Mhasibu na mlezi katika Seminari ndogo ya Mtakatifu Francis, Kasita. Kati ya mwaka 2005-2009 alitumwa katika Chuo kikuu cha Duquesne huko Pittsburgh, Pennsylvania Marekani ambako alitunikiwa shahada ya Uzamili katika Falsafa. Mwaka 2009-2014 alikuwa Gombera wa Seminari ndogo ya Mtakatifu Francis, Kasita. Na tangu mwaka 2014 amekuwa Paroko wa Kanisa kuu Kwiro na Dekano. Tangu mwaka 2015 alikuwa ni Mkurugenzi wa Shule ya Sekondari ya Mtakatifu Yosefu na Mwenyekiti wa Umoja wa Mapadre Wazalendo (UMAWATA) Jimboni Mahenge.

Tarehe 8 Desemba 2018, Baba Mtakatifu Francisko akamteua kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la TUNDURU-Masasi, Ili kuziba nafasi iliyoachwa wazi kutokana na kifo cha Mhashamu Askofu Castor Msemwa aliyeliongoza Jimbo hili kuanzia mwaka 2005 hadi mwaka 2017 alipofariki dunia! Jimbo lina parokia 19 zinazohudumiwa na Mapadre wa Jimbo 24, Wasalvatoriani 14 na Mapadre kutoka majimbo mengine ya Tanzania ni 3. Kuna Parokia 2 teule, yaani Parokia ya Magumuchila na Chikunja, zinazotarajiwa kupewa hadhi na kuwa Parokia kamili.

KIAPO CHA UAMINIFU: Mimi Padre Filbert Felician Mhasi, niliyeteuliwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la TUNDURU – Masasi, nitakuwa daima mwaminifu kwa Kanisa Katoliki na kwa Askofu wa Roma, ndiye Mchungaji wake Mkuu, tena wakili wa Kristo, Halifa wa Petro Mtume katika ukulu wake. Nitakuwa pia mwaminifu kwa urika wa Maaskofu. Nitajali utekelezaji huru wa mamlaka makuu ya Papa kuhusu Kanisa ulimwenguni kote. Tena nitajibidisha kuhifadhi na kupigania haki na madaraka yake. Nitazitambua na kuzilinda haki za nyadhifa za wajumbe wa Askofu wa Roma, kwa maana hao huwakilisha nafsi ya Mchungaji Mkuu mwenyewe.

Nitajitahidi kwa bidii kubwa kuzitekeleza kazi walizokabidhiwa Maaskofu, yaani, kulifundisha Taifa la Mungu, kulitakatifuza na kuliongoza. Haya nitayafanya nikiunganika na kichwa cha urika wa Maaskofu, nikiunganika pia na Maaskofu wengine wote katika umoja wa hierakia. Nitaulinda Umoja wa Kanisa ulimwengu. Kwa hiyo nitajishughulisha kwa bidii ili hazina ya imani, tuliyoipata kutoka kwa Mitume, itunzwe safi na kamili. Nitautunza pia ukweli ulio wa lazima kusaidiwa na kutekelezwa kimaadili. Huo ukweli nitauangalia ufundishwe na uelezwe kwa wote, kama anavyoeleza Mwalimu Mama Kanisa. Lakini waliopotoka katika ukweli nitawaonesha moyo wangu wa kibaba na nitatumia misaada yote mpaka waufikie ukamilifu wa ukweli Katoliki.

WOSIA KWA ASKOFU MPYA: Ndugu wapendwa, fikirini kwa makini ni daraja gani anayopewa huyu ndugu yetu katika Kanisa. Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetumwa na Baba ili kuwakomboa wanadamu, naye mwenyewe aliwatuma duniani Mitume thenashara, ili baada ya kujazwa nguvu ya Roho Mtakatifu, waihubiri Injili na wakiwakusanya watu wote katika zizi moja, wawatakatifuze na kuwaongoza. Lakini ili utume huo upate kuendelea mpaka ukamilifu wa dahari. Mitume waliokuwa wamepewa na Kristo kwa kuwawekea mikono, wamelipokea kutoka kwa Kristo; na kwa tendo hilo hutolewa utimilifu wa Sakramenti ya Daraja. Ndivyo toka kizazi hata kizazi, kwa njia ya urithi usiokatizwa wa Maaskofu, umeendelezwa hapa duniani utume ulikabidhiwa na Kristo kwa Mitume, na kazi ya mwokozi inaendelea na kustawi hadi nyakati zetu.

Katika nafsi ya Askofu anayezungukwa na mapadre wake, yupo kati yenu Bwana wetu Yesu Kristo milele. Maana katika huduma ya Askofu, Kristo mwenyewe anaendelea kuihubiri Injili na kuwagawia waamini mafumbo ya Imani. Tena katika ubaba wa Askofu, yeye mwenyewe anauongezea mwili wake viungo vipya na kuviunganisha. Yeye mwenyewe katika hekima na busara ya Askofu, ndiye mwenyewe awaongozaye ninyi katika hija ya hapa duniani hadi kuifikia heri ya milele. Hivyo basi, mpokeeni kwa moyo wa shukrani na furaha huyu ndugu yetu ambaye sisi Maaskofu, kwa kumwekea mikono, tunamwunganisha katika urika wetu.

Tena mheshimuni kama mtumishi wa Kristo na mgawaji wa mafumbo ya Mungu, maana yeye amekabidhiwa ushuhuda wa Injili ya ukweli na huduma ya Roho Mtakatifu na ya haki.Nanyi yakumbukeni maneno ya Kristo asemaye na Mitume; “Awasikilizaye ninyi, anisikiliza mimi, naye awakataaye ninyi, anikataa mimi, naye anikataaye mimi, amkataa yeye aliyenituma”. Nawe ndugu mpendwa, uliyeteuliwa na Bwana, uzingatie moyoni kuwa umechaguliwa kati ya wanadamu ukawekewa kwa ajili ya wanadamu katika mambo yamhusuyo Mungu. Maana Uaskofu ni jina linalomaanisha utumishi wala si adhama, na Askofu hupaswa kutumikia kuliko kutawala; kwa sababu, kadiri ya maagizo ya mwalimu wetu: “aliye mkubwa na awe kama aliye mdogo, na mwenye kuongoza kama yule atumikiaye”.

Lihubiri Neno wakati ufaao na wakati usiofaa, onya kwa uvumilivu wote na mafundisho. Usiache kuomba kutoka katika utimilifu wa utakatifu wa Kristo wingi wa neema mbalimbali kwa ajili ya watu waliokabidhiwa. Uwe mgawaji wa mafumbo ya Kristo, msimamizi na mlinzi mwaminifu katika Kanisa ulilokabidhiwa. Uliteuliwa na Baba ili uiongoze familia yake, basi umkumbuke daima Mchungaji mwema, ambaye anawajua kondoo zake, nao wanamjua; nay eye hakusita kuutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo wake. Uwapende wote anaokukabidhi Mungu kwa Upendo wa kibaba na kindugu; kwanza Mapadri na Mashemasi washiriki wako katika utumishi wa Kristo; lakini pia walio maskini na wadhaifu, wasafiri na wageni. Uwahimize waamini wote washirikiane nawe katika kazi ya kitume, wala usikatae kuwasikiliza kwa radhi. Aidha, kuhusu wale ambao hawajaingizwa bado katika zizi lile moja la Kristo, nao uwashughulikie bila kuchoka, maana hao nao wamekabidhiwa kwako na Bwana.

Katika Kanisa Katoliki linalokusanyika kwa kifungo cha Upendo, wewe umeunganika katika urika kwa maaskofu, hivi kwamba usiache kujishughulisha na Makanisa yote; nawe uyabuni kwa moyo radhi Makanisa yanayohitaji zaidi msaada. Hatimaye ulitunze kundi zima ambapo Roho Mtakatifu amekuweka ili ulisimamie Kanisa la Mungu; ulitunze kwa jina la Baba ambaye katika Kanisa wewe usura yake’ na kwa jina 46 la mwana wake Yesu Kristo ambaye unapewa wadhifa wake wa kuwa Mwalimu, Kuhani na Mchungaji; kwa jina la Roho Mtakatifu anayelihuisha Kanisa la Kristo na kututegemeza sisi katika udhaifu wetu kwa nguvu yake.

MASHIRIKA YA KITAWA YANAYOFANYA KAZI JIMBONI

Shirika la MUNGU MWOKOZI “The Society of the Divine Savior SDS” – Salvatorians. Limeanza kufanya kazi toka mwanzo wa jimbo la Nachingwea hadi sasa jimbo la TUNDURU-Masasi. Nao wapo makundi mawili. Mapadre na Mabruda ambao wana nyumba yao kuu Masasi mjini eneo la Migongo. Pia wana nyumba ya malezi kwa waombaji na wapostolanti Namiungo na wanovisi Nakapanya katika wilaya ya Tunduru. Pia wanafanya kazi za kitume katika parokia tano Jimboni humu! Masista Wasalvatoriani nao walianza kufanya kazi za kitume toka jimbo la Nachingwea. Wao wana makao makuu yao Masasi, Migongo. Wana nyumba ya malezi kwa wakandidati Naluale wilaya ya Tunduru na wanovisi katika nyumba ya malezi Makulani wilaya ya Masasi. Wanafanya kazi za kitume kwenye parokia 5.

Masista Wabenediktini wa Shirika la Bikira Maria Msaada wa Wakristo Ndanda. Hawa wanafanya kazi parokia ya Nambaya wilaya ya Masasi. Wapo pia Masista Wabenediktine wa Mtakatifu Agnes kutoka Chipole- Songea. Kundi moja linatoa huduma uaskofuni Tunduru na wengine parokia ya Kanisa Kuu. Kuna Masista wa Maria Imakulata (SMI). Hawa wana nyumba mbili. Moja iko Nanjota ambako wana nyumba ya malezi kwa waombaji na wapostolanti. Pia wanashughulikia vijana, chekechea, na zahanati. Pia wana nyumba ya malezi parokia ya Chikukwe kwa wanovisi. Hapa wanashughulikia chekechea, na vijana. Nyumba zote mbili ziko katika wilaya ya Masasi. Shirika la Bikira Maria Malkia wa Mitume Mbeya- Waliwasili jimboni Januari 6, 2018 wanafanya kazi Seminari ya Muhuwesi.

HUDUMA: AFYA: Jimbo lina kituo cha Afya kimoja na zahanati 7, ili kukoleza uinjilishaji wa kina jimbo linapeleka vijana vyuo vya katekesi vilivyo majimbo ya jirani, ili parokia ziwe na makatekista wenye elimu na katekesi makini. Pia karibu kila parokia inashughulika kujenga makanisa ya vigango na pengine makanisa makubwa ya parokia pale ambapo makanisa ya zamani ni madogo kukidhi idadi ya waamini kwa wakati huu.

ELIMU: Jimbo lina shule moja ya VETA, kwa mafunzo ya useremala, ushonaji, mapishi na kompyuta. Walau kila parokia ina shule ya malezi kwa watoto chekechea. Jimbo lina Seminari ndogo ya Mtakatifu Dionisius katika kijiji cha Muhuwesi umbali wa km 25 kutoka Tunduru mjini kuelekea Masasi.


Maoni


Ingia utoe maoni