Dhamana na utume wa wana tasnia ya mawasiliano ya jamii ni sehemu ya mchakato wa kujenga na kudumisha jumuiya inayofumbatwa katika mawasiliano, kwa kukazia ukweli na mafungamano ya kijamii; kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa majadiliano na kusikilizana; kwa kuunganisha na kamwe mawasiliano yasiwe ni kwa ajili ya kuwatenganisha na kuwasambaratisha watu. Mitandao ya kijamii iwe ni madaraja ya kuwakutanisha watu!
Kwa ufupi, hiki ndicho kiini cha ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya 53 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni kwa mwaka 2019, itakayoadhimishwa na Mama Kanisa hapo tarehe 2 Juni 2019. Baba Mtakatifu anawaalika na kuwahamasisha wadau katika tasnia ya mawasiliano ya jamii kuuvua uongo na kusema ukweli kwa maana wao ni viungo, kila mmoja kiungo cha mwenzake. (Rej. Ef. 4:25). Bwana Brad Smith, Rais wa Kampuni ya Microsoft, katika mahojiano na Andrea Monda, Mkurugenzi wa Gazeti la L’Osservatore Romano, kwa namna ya pekee kabisa, amekazia mawazo ya Baba Mtakatifu Francisko anayependa kuona kwamba, mitandao ya kijamii inakuwa ni madaraja ya kuwakutanisha watu, ili kutambua na kuthamini uwepo wa kila mtu.
Ikiwa kama mitandao ya kijamii itatumika kama daraja na matumaini ya kuwakutanisha watu, basi hapo itakuwa imetekeleza dhamana na wajibu wa kujenga jumuiya inayoheshimiana na kuthaminiana. Maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ni muhimu sana, ikiwa kama yatasaidia mchakato wa kukuza na kudumisha umoja na mafungamano ya kijamii; kanuni maadili na utu wema; siasa shirikishi pamoja na haki. Katika ulimwengu huu ambamo watu wanathamini sana takwimu, kuna haja ya kuhakikisha kwamba, utu, heshima na haki msingi za binadamu zinaheshimiwa na kuthaminiwa.
Bwana Brad Smith, anasema, matumizi ya“Artificial Intelligence” yaani “akili bandia”yanaendelea kuleta mageuzi makubwa katika ulimwengu wa kazi na mahali wanapoishi watu! Mabadiliko haya ni makubwa, kumbe, yanapaswa kuongozwa na kusimamiwa na sheria mpya, kanuni maadili na utu wema. Katika mchakato wa tasnia ya mawasiliano, kuna haja ya kusikiliza sauti ya kiongozi kama Papa Francisko anayekazia: huruma na upendo, udugu na mshikamano. Maendeleo ya sayansi na teknolojia yanachangia kwa kiasi kikubwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, lakini hayana budi kufumbatwa katika utu na heshima ya binadamu.
Microsoft Word ni chombo cha huduma ambacho kimetumiwa na watu wengi kwa ajili ya maendeleo, lakini pia, kuna baadhi ya watu wamekitumia vibaya kwa malengo yao binafsi kiasi cha kuleta tafrani ulimwenguni. Sayansi na teknolojia haina budi kujikita katika misingi ya maadili na utu wema; malezi na majiundo kwa ajili ya matumizi sahihi ya nyenzo za mawasiliano ya jamii; ili kujenga uelewa na uwajibikaji wa pamoja. Matumizi ya “akili bandia” yataendelea kusababisha mabadiliko makubwa katika maisha ya watu, kumbe, malezi na majiundo makini ni muhimu sana hasa kwa vijana wa kizazi kipya.
Hili ni jukumu la viongozi wa Serikali, wanasiasa, watunga sera na sheria; wafanyabiashara, wasomi na wanazuoni pamoja na viongozi wa dini kushirikiana na kushikamana, ili kuhakikisha kwamba, utu, heshima na haki msingi za binadamu zinalindwa na kudumishwa. Kwa njia hii, wataweza kugundua mapungufu yanayoweza kujitokeza na hivyo kuyafanyia kazi kwa kuangalia mambo msingi yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza. Microsoft Word ina tambua dhamana na wajibu wake katika kukuza na kudumisha kanuni auni kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Ndiyo maana, imekuwa ikichangia rasilimali fedha kwa ajili ya kukuza na kuendeleza teknolojia ya mawasiliano sehemu mbali mbali za dunia.
Ni Kampuni inayowekeza zaidi katika teknolojia rafiki, inayoweza kutumiwa na wengi, kwa kuzingatia na kuheshimu faragha ya watu; kwa kukuza na kudumisha usalama, umoja, mshikamano na udugu. Microsof Word inaendelea kuchangia rasilimali fedha ili kuwajengea watu uelewa na matumizi sahihi ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano; walengwa wakuu ni wanafunzi wanaotoka katika mazingira magumu na hatarishi. Vinginevyo, vijana wanaotoka katika maeneo haya wataendelea kubaki nyuma ya teknolojia. Maendeleo ya teknolojia yalenge ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Uwajibikaji wa wote, kanuni maadili na utu wema; utawala wa sheria na haki ni mambo msingi katika kukuza matumizi halali ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ya jamii.
Kwa njia ya Mfumo wa “Digital Civilicity Index” Yaani “Kipimo cha Mfumo wa Ustaarabu wa Kidigitali”, kinaonesha kwamba, madhara ya mitandao ya kijamii yanagusa na kupekenya uhalisia wa maisha ya watu. Microsoft Word inaendelea kuboresha mawasiliano, ili kuwasaidia wadau mbali mbali kutumia kwa heshima na adabu mitandao ya kijamii. Kuna watu wengi wameathirika sana kutokana na matumizi haramu ya mitandao ya kijamii, kiasi hata cha kujinyonga. “Digital Civility Challenge” yaani “Mfumo wa Changamoto ya Ustaarabu wa Kidigitali, kinawaamasisha wadau mbali mbali kutumia vyema mitandao ya kijamii; kwa kuhakikisha usalama, utu na heshima yao.
Maoni
Ingia utoe maoni