Baba Mtakatifu katika mahubiri yake, amewataka wazazi, walezi na wasimamzi wa Ubatizo kuhakikisha kwamba, wanawarithisha watoto wao imani ya Kanisa, kwa kuanzia na ushuhuda wa imani toka ndani ya familia ambako watoto wanaanza kujifunza mambo msingi ya maisha, na baadaye kuendelea na katekesi ya kina utakapofika wakati wake!
Maadhimisho ya Siku kuu ya Ubatizo wa Bwana, yanafunga rasmi shamra shamra zote za Liturujia ya Kipindi cha Noeli. Katika Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Kikanisa cha Sistina, kilichoko mjini Vatican, Jumapili tarehe 13 Januari 2019 ametoa Sakramenti ya Ubatizo kwa watoto wachanga 27, kati yao watoto wa kiume ni 12 na wa kike ni 15 walioandaliwa, ili waweze kuzaliwa upya kwa “Maji, Roho Mtakatifu na katika Neno” tayari kushiriki: Ufalme, Ukuhani na Unabii wa Kristo Yesu.
Baba Mtakatifu katika mahubiri yake, amewataka wazazi, walezi na wasimamzi wa Ubatizo kuhakikisha kwamba, wanawarithisha watoto wao imani ya Kanisa, kwa kuanzia na ushuhuda wa imani toka ndani ya familia ambako watoto wanaanza kujifunza mambo msingi ya maisha, na baadaye kuendelea na katekesi ya kina utakapofika wakati wake! Lakini, familia ni chemchemi na shule ya imani kwa watoto! Hii ndiyo imani ambayo wazazi na wasimamizi wa Ubatizo wameomba kwa Kanisa, ili kwa njia ya imani watoto hawa waweze kumpokea Roho Mtakatifu anayewakirimia neema ya utakaso wa dhambi na hivyo kuzaliwa upya katika Roho Mtakatifu; tayari kupokea Mapaji ya Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu anawaachia chapa ya kudumu katika nyoyo zao.
Baba Mtakatifu anakaza kusema, familia inapaswa kuwa ni mahali pa kwanza pa kurithisha imani. Baadaye watoto hawa wataweza kupata nafasi ya kuendelea kujifunza Katekisimu ya Kanisa ambayo kimsingi ni muhtasari wa: Imani, Sakramenti za Kanisa, Maisha Adili na Maisha ya Sala. Shuleni na Parokiani wataweza kujifunza mambo haya kwa kina, lakini familia ndiyo chimbuko la imani inayofumbatwa katika ushuhuda wa upendo unaomwilishwa katika maisha ya kifamilia, katika lugha inayofahamika na watoto wenyewe na hatimaye, watoto wanaweza kujifunza pia kutoka katika jamiii inayowazunguka.
Ikumbukwe kwamba, imani inarithishwa kwanza kabisa kwa njia ya maneno na matendo; kwa kuwafundisha watoto kufanya Ishala ya Msalaba, muhtasari wa Fumbo la Utatu Mtakatifu. Hili ni zoezi ambalo linakwenda sanjari na dhamana pamoja na wajibu wa wazazi kwa watoto wao, yaani kulea uzima ambao Mwenyezi Mungu amewaamisha. Baba Mtakatifu anaonya kwamba, leo hii kuna watoto ambao hawajui kufanya Ishala ya Msalaba hata kidogo! Kumbe, wajibu wa kwanza wa wazazi ni kuwafundisha watoto wao kufanya Ishala ya Msalaba.
Imani inapaswa kumwilishwa katika matendo ya huruma na mapendo, kama sehemu ya mchakato utakaowawezesha wazazi kurithisha imani hii kwa watoto wao. Familia inapaswa kuwa ni Kanisa dogo la nyumbani, mahali ambapo upendo kati ya Bwana Bibi unadhihirishwa wazi; mahali ambapo amani na utulivu vinamwilishwa katika uhalisia wa maisha na kwa njia hii, watoto wataweza kugundua uwepo endelevu wa Kristo Yesu ndani ya familia yao. Wazazi waepukane na kishawishi cha kupigana au kutoleana maneno makali mbele ya watoto wao! Kwa hakika, kukosa na kukoseana ni sehemu ya maisha ya watu wa ndoa. Huu ni ukweli ambao kamwe hauwezi kufumbiwa macho anasema Baba Mtakatifu!
Lakini, jambo la kutilia mkazo ni kwamba, wazazi wanapotaka kurekebishana wafanye zoezi hili pasi na uwepo wa watoto wao, kwani watoto wanapowaona wazazi wao “wakirushiana masumbwi na maneno mazito mazito” watoto wanateseka sana nyoyoni mwao. Kwa kufanya mambo haya faraghani, wazazi hata katika udhaifu wao wa kibinadamu, bado wataendelea kuwa ni vyombo na mashuhuda wa kurithisha imani kwa watoto wao.
Baba Mtakatifu amewapatia akina mama waliokuwa wananyonyesha, “ruksa” ya kuwanyonyesha watoto wao pengine wanasikia baridi, njaa au ishala fulani kwa wazazi wao. Inafurahisha kusikiliza kwaya ya watoto wachanga wanaowalilia wazazi wao, ili wapate kuwanyonyesha, mara nyingi iki ni kilio kinachoanzishwa na mtoto mmoja na wengine wanaitikia na hivyo kuwa wimbo wa sifa kwa Mwenyezi Mungu, chemchemi ya uhai wa mwanadamu! Sakramenti ya Ubatizo unawakirimia waamini maisha ya uzima wa milele yanayopata chimbuko lake kutoka katika Fumbo la Umwilisho linalokamilika katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu!
Maoni
Ingia utoe maoni